MACHAFUKO makubwa yameukumba mji wa Zanzibar juzi na jana, ambapo kanisa moja limelipuliwa na kitu kinachoaminika kuwa bomu la kurusha kwa mkono, huku kukiwa na madai kuwa Watanzania wenye asili ya Bara wanaoishi na kufanya kazi visiwani hapa wameshambuliwa.
Mashuhuda wameliambia Tanzania Daima kwamba, watu ambao hadi sasa hawajajulikana, lakini wakiaminika kuwa ni wafuasi wa kundi la kidini la uamsho, walilishambulia na kulilipua Kanisa la Tanzania Assemblies of God la Kariakoo, visiwani hapa kuharibu magari, miundombinu na mali nyingine.
Taarifa hizo zilizothibitishwa na Jeshi la Polisi, zimesema kuwa, wafuasi wa kundi hilo walianza vurugu hizo juzi, wakipinga kitendo cha kukamatwa kwa kiongozi wao, Mussa Juma kwa kosa la kufanya maandamano bila kibali cha polisi.
Habari zimedai kuwa, baada ya kukamatwa kwa kiongozi huyo, wafuasi wake walianza kuhamasishana kwenda Kituo cha Polisi Madema, kilichoko Wilaya ya Mjini Magharibi wakiwa na silaha za mawe, jambo lililowafanya polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.
Hata hivyo, habari zinadai kuwa, baada ya kutawanyika, majira ya saa mbili usiku wafuasi hao walianza kuziba barabara kwa mawe na magogo makubwa, kuchoma matairi katika maeneo ya Michenzani, kabla ya kuyashambulia na kuyaharibu vibaya magari kadhaa.
Aidha, mashuhuda wamedai kuwa, baadhi ya wafuasi hao walianza kuzisaka nyumba za ibada na ndipo walipokwenda lilipo kanisa hilo, na kuanza kulishambulia kwa mawe, kabla ya kulilipua kwa kitu kinachoaminika kuwa bomu.
Kadhalika, kuna madai kuwa wafuasi wengine wa kundi hilo, walijigawa na kuanza kuzifuatilia nyumba wanamoishi wafanyabiashara na wafanyakazi wanaotoka Tanzania Bara na kuzishambuli kwa mawe, huku wakitoa maneno ya vitisho.
Mmoja wa wafanyakazi hao kutoka Bara, anayefanya kazi katika hoteli moja ya kitalii (jina linahifadhiwa), alikiri nyumba yao kushambuliwa vikali, na jana alilazimika kuhamia kwa rafiki zake ambao ni wenyeji wa visiwani hapa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Musa Ali katika taarifa yake jana kwa vyombo vya habari, amekiri kuharibiwa kwa kanisa hilo, na kwamba hadi jana mchana watu saba walikuwa wakishikiliwa na jeshi hilo.
Kamishina Ali alisema, kundi hilo katika mwendelezo wake wa kufanya mikusanyiko kwa ajili ya makongamano, mihadhara, dua na itkafu, juzi lilikuwa katika viwanja vya Lumumba majira vya asubuhi kwa dhamira ya kusasababisha watu wauchukie Muungano na kuitaka serikali iitishe kura ya maoni kuhusu kuendelea, au kutoendelea kwa Muungano na serikali zake.
Alisema pamoja na kufanya matendo mengine ya uvunjifu wa amani kinyume na lengo la kuanzishwa kwa jumuia hiyo na katiba yao, majira ya saa za mchana viongozi wao waliwahamasisha watu waliokuwa katika kongamanao hilo kufanya maandamano bila kuarifu polisi.
Kamishna Ali alidai, kutokana na historia ya nyuma ya kundi hilo, polisi walilazimika kuyavunja kwa vile katika siku za karibuni jumuiya hiyo ilikwishaonesha dalili za uvunjifu wa amani kwa kufanya matendo mbalimbali, ikiwemo kutoa lugha ya matusi kwa viongozi wa serikali na wananchi ambao hawakuwaunga mkono.
Alisema kundi hilo limekuwa likifunga barabara bila sababu, kutembea na ving’ora isivyo halali, kuwashambulia watu kwa silaha zenye ncha kali, kuharibu mali za watu kama magari, na vingine vya aina hiyo.
Kutokana na tukio hilo, polisi wametangaza msako mkali wa viongozi na wanaokifadhili kikundi hicho kwa gharama yoyote, na waliohusika na vurugu hizo na kwamba watakaopatikana watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka.
Kamishna huyo amesema polisi na vikosi vya usalama wameimarisha ulinzi kuhakikisha kuwa usalama wa maisha ya watu na mali zao unadumishwa kwa gharama yoyote.
CHADEMA wailaumu serikali
Jijini Dar es Salaam, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema Rais Jakaya Kikwete, Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na CCM wamesababisha mivutano na vurugu Zanzibar kwa kutaka kudhibiti mjadala kuhusu muundo wa muungano na uhuru wa nchi katika mchakato wa katiba mpya kwenye suala hilo tete na tata.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Habari wa Uenezi wa chama hicho, John Mnyika ambaye alisema mivutano na vurugu zinazoendelea Zanzibar ni matokeo ya Serikali ya Muungano na ya Mapinduzi Zanzibar kutokuzingatia mapendekezo ya chama hicho kuhusu umuhimu wa uhuru wa mjadala kuhusu muundo wa muungamo katika mchakato wa katiba mpya.
Aidha, alisema mvutano huo umeshika kasi baada ya maamuzi ya NEC ya CCM bila ya maoni ya wanachama wake wa Zanzibar na Tanzania Bara kuminya mjadala kuhusu suala hilo.
|
No comments:
Post a Comment
hey! whats up! we are happy to attend that lever we need your help by contribute with idea and other things. thank you